Breaking

Thursday, 17 March 2022

WATU 14 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUSAMBAZA VIDEO YA MGONJWA ALIYELAZWA ICU MUHIMBILI

 



Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) linawashikilia watu 14 kwa tuhuma za kusambaza video katika mitandao ya kijamii kinyume na sheria ikimuonyesha mmoja wa wagonjwa (Polisi hawajamtaja jina) aliyekuwa amelazwa wodi ya ICU Hospitali ya Taifa ya Muhimbili suala lililoleta taharuki kwa Hospitali hiyo na Wafanyakazi wake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ACP Muliro Jumanne amesema kuwa watuhumiwa hao akiwemo Allen Samuel Mhina ( 31), Mkurugenzi wa Mtandao wa kijamii wa U-turn Collection mkazi wa Temeke Mwembeyanga na wenzake 13 walikutwa na vifaa mbalimbali vya kieletroniki vya kiuchunguzi ambavyo ni Kamera, Kalamu, Saa Funguo, Miwani, Kofia, Laptop, Memory Card ambavyo vyote vinachunguzwa.

"Kitendo kinachotuhumiwa kufanywa na watuhumiwa hao kililenga kudhalilisha, kutia hofu au kuleta taharuki suala ambalo linalazimisha mamkala hizi mbili za kisheria kuchunguza kwa kina suala hilo, uchunguzi ukikamilika watafikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria" amesema Kamanda muliro

Itakumbukwa hivi karibuni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi alisema vyombo vya dola vinafanya uchunguzi kubaini aliyemrekodi Prof. Jay (ICU) na akaagiza Hospitali zote nchini kuweka matangazo yanayokataza kupiga picha bila kibali.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages