Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria walimu watakaobainika kudai malipo kwa wanafunzi akisema elimu ni bure.
RC Mjema ametoa agizo hilo Alhamisi Machi 03, 2022 wakati akifungua kikao cha Wadau wa elimu Mkoa wa Shinyanga chenye lengo la kujadili maendeleo ya elimu ili kuboresha elimu Mkoani humo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa.
Amesema kuwa mwalimu yeyote atakayebainika kuchangisha fedha achukuliwe hatua kwani kumekuwa na upotoshaji kuwa wazazi wanatakiwa kulipa ada.
Ameongeza kuwa shule za serikali na za binafsi za mkoa wa Shinyanga zinatakiwa kushikamana ili kusimamia elimu bora na kuziwezesha kuingia katika nafasi ya 10 bora kitaifa.
"Tunachokwenda kufanya sasa ni kuboresha mazingira yaliyopo shuleni Wote tunatakiwa tushikamane, upande wa shule binafsi na za serikali. Tunataka shule zetu ziingie kumi bora kitaifa kila mwaka" amesema
Aidha amewataka Wakurugenzi kuwawekea walimu mazingira mazuri ya kazi ikiwemo kuwapa nyumba za kuishi hali itakayochochea ufaulu kuongezeka.
Kwa upande Mwingine Amewataka Wakuu wa wilaya kwenda kusimamia upatikanaji wa chakula shuleni ili wanafunzi wawe na lishe bora na kuongeza morari ya kujisomea hali itakayochangia kuongeza ufaulu.
"Tukasimamie pia mdondoko, watoto wafuatiliwe wako wapi, watoto wanatakiwa wawe shule kama tulivyowaandikisha, tusikubali kuwa chini ya asilimia 100,”amesema Mjema.