Breaking

Monday, 21 March 2022

WAKUU WA MIKOA WATAKIWA KUSIMAMIA ONGEZEKO LA MAPATO KWENYE HALMASHAURI

 



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungaa amewataka wakuu wa Mikoa kuongeza usimamizi katika kuhakikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye Halmashauri unaongezeka kupitia vyanzo mbalimbali.


Waziri Bashungwa ameyasema hayo wakati wa kikao kazi cha kupitia Sura ya Mipango na Bajeti ya OR- TAMISEMI, Tume ya Walimu, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka 2022/23 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma.


Amesema, ni vyema kikao hicho kikatumika kujadili masuala yote ya msingi ambayo yatawawezesha kufanikisha utekelezaji wa Mipango na Bajeti katika maeneo yao.


"Nategemea kuona michango mingi ikielekezwa katika kusimamia na kuongeza mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kusimamia utoaji wa huduma bora za jamii na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati katika halmashauri zetu ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi na kuinua mapato ya ndani ya halmashauri zetu,"amesisitiza.



Aidha, Waziri Bashungwa aliongeza kuwa hawawezi kufanikisha azma ya Serikali na wananchi ya kuwaletea maendeleo kwa kutoa huduma bora za afya, elimu bila malipo, huduma bora ya maji safi na salama, miundombinu ya barabara kama Serikali haiwezi kukusanya mapato ya kutosha kugharamia huduma hizo.


Waziri Bashungwa amesema  ni wajibu wetu kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha kuwa vyanzo mbalimbali na vya uhakika vya kuongeza mapato katika maeneo yetu vinabuniwa na kuendelezwa kwa kuwekewa utaratibu wa kisheria ili viweze kutumika kuzalisha mapato.


"Ni vyema vyanzo vya mapato vilivyopo vikaendelea kuboreshwa, mifumo madhubuti ya ukusanyaji mapato ukatumika kikamilifu ili kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali," amesema.




Pia, Waziri Bashungwa amesema Serikali imekuwa ikiimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali.


"Ni jukumu letu sote kwenda kusimamia matumizi ya mifumo hiyo na changamoto zozote mtakazokuwa mnazibaini zitolewe taarifa ili maboresho yaendelee kufanyika,"amesema Waziri Bashungwa.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages