Breaking

Friday 18 March 2022

UKATILI DHIDI YA WATOTO MTANDAONI WAPATIWA UFUMBUZI

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis(wa tatu kushoto) akionesha nakala ya Taarifa ya utafiti wa Hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni baada ya kuzindua taarifa hiyo jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake ma Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitoa kwa baadhi ya wadau, nakala ya taarifa ya utafiti kuhusi hali ya ukatili mtandaoni dhidi ya watoto, baada ya kuizindua taarifa hiyo, jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/0/2022.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku akieleza lengo la uzinduzi wa Taarifa ya utafiti wa hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni, jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022.


Mwakilishi wa Shirika la umoja wa Mataifa la Unicef Shalini Baghuna akitoa  maelezo kuhusu taarifa ya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni wakati wa uzinduzi wa taarifa hiyo uliofanyika jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022.

Baadhi ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wa taarifa ya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni wakifuatilia matukio mbalimbkai katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii akiwa na Viongozi  wa baraza la watoto (kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza )Nancy kasembo na (kutoka Kulia ni Makamu mwenyekiti)Godlisten Boniphace. Pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Unicef Shalini Bahguna (Wa pili kutoka kushoto mwa Naibu Waziri),Pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Ecpact Yusta Mwaituka (wa tatu kushoto kutoka Naibu Waziri) na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo Ya Mtoto ,Sebastian Kitiku (Wa pili kulia kutoka kwa Naibu Waziri) katika Uzinduzi wa taarifa ya utafiti kuhusu hali ya ukatili wa watoto mitandaoni uliofanyika jijini Dar es salaam leo tarehe 18/03/2022


***********

Na Mwandishi Wetu 


Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,  Mwanaidi Ali Khamis ameitaka jamii kuwaepusha watoto dhidi ya madhara ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ili kuepukana na ukatili mtandaoni ikiwemo wa ukatili wa kingono. 


 Mwanaidi ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 18, 2022 alipokuwa akizindua Taarifa ya Utafiti kuhusu Hali ya ukatili Dhidi Ya Watoto Mtandaoni, uliofanyika Jijini Dar es Salaam.


Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo yote ya ulinzi  kama ilivyoelekezwa katika Mikataba ya kikanda na Kimataifa kuhusu haki na Ustawi wa Mtoto ili kumlikdatoto na vitendo vya ukatili ikiwemo ukatili mtandaoni.


“Tutaendelea kusimamia Sera na Sheria mbalimbali zinazomhusu Mtoto na kuandaa miongozo inayohitajika ili kuhakikisha  kwamba hakuna mtoto anayefanyiwa ukatili" amesema Mhe. Mwanaidi.


Ameongeza kuwa amefarijika kupata taarifa ya hali ya ukatili wa kimtandao katika kipindi hiki ambapo tumeanza kushuhudia watoto wameanza kupata madhara yanayotokana na ukatili wa kimtandao nchini hivyo itasaidia kuongeza afua zaidi za kupambana na ukatili mtandaoni ambao unaonea kwa kasi.


"Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia matumizi makubwa ya vifaa vya kielektroniki hasa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo vifaa hivyo vimekuwa kiungo muhimu kwa ajili ya mawasiliano kwenye kuendesha vikao mbalimbali" amesema Mhe. Mwanaidi 


Mhe. Mwanaidi ameeleza kuwa taarifa ya utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto Mtandaoni uliofanyika mwaka 2018 na Mtaalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt Hezron Onditi inaonyesha kuwa asilimia 4 ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 17 walifanyiwa ukatili wa kingono ikiwemo kulazimishwa kutoa picha zao za utupu.


"Pamoja na faida nyingi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa, tumeshuhudia matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii yakihusisha zaidi kundi la watoto na vijana balehe" amesema Mhe. Mwanaidi


Akieleza lengo la utafiti huo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto Sebastian Kitiku  amesema matumizi ya vifaa mbalimbali vya kielekroniki yamekuwa yakitumika kwa wingi, hivyo kumekuwa na changamoto ya kutaka kujua ukubwa wa tatizo hilo. Hivyo, Serikali kwa kishirikiana na wadau wakaona ni vema kufanya utafiti huo.


“Utafiti umetumia mbinu mbalimbali kama uchambuzi wa Sera na Sheria zilizopo Nchini ,Upitiaji wa nyaraka mbalimbali mitandaoni,Mahojiana na Watoto na Wazazi  kwa ujumla Pamoja na Mikusanyiko mbalimbali kwa kushirikiana na ngazi za kata hadi mkoa.”amesema Kitiku.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto Nancy Kasembo ameshukuru kwa kushirikishwa kwao katika michakato inayowahusu watoto kwani ina manufaa kwao na kuiomba jamii kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa watoto katika mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.


“Watoto hawajui namna ya kutoa taarifa baada ya kufanyiwa ukatili,aidha bado kuna unyanyapaa dhidi ya wahanga wa ukatili hivyo kupelekea wahanga kutotoa taarifa”. amesema Nancy


Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Unicef  Shalini Bahguna ameipongeza Serikali kwa kuweka juhudi za msingi za kupinga vikali ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hasa katika jitihadaz.a kupambana na ukatili mtandaoni.


Amesema Shirika hilo limejikita katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama na kuhakikisha watoto wanajengewa uwezo wa kujitambua ili kuepukana na ukatili wa mtandaoni na kuiomba Serikali kuendelea kutoa ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuondoa  tatizo  la Ukatili mitandaoni.


Baadhi ya wadau wakichangia umuhimu wa utafiti huo wamesema ni vema kuwekeza kwenye kuweka mbinu zinazozuia watoto kufanyiwa ukatili wa mitandaoni kabla haujatokea na hiyo ni kwa mbinu kama kuzuia na kuwakataza watoto kujihusisha na baadhi utumiaji wa mitandao kama watu wazima.


Aidha, wameiomba Serikali  kuwajengea uwezo watoa huduma  hususani kwenye madawati ya kijinsia na Polisi na kuwaasa wazazi na walezi  kujadili masuala ya msingi yanayowahusu watoto wao ili kuwajengea ukaribu na watoto waweze kusema pale wanapofanyiwa ukatili.


MWISHO

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages