Shirika la Viwango Tanzanaia (TBS) Kanda ya Magharibi limewakamata wafanyabiashara 36 kwa makosa ya kuuza bidhaa zilizoisha muda wa matumizi ( expired date) pamoja na kuuza bidhaa ambazo zimeshapigwa marufuku.
Akizungumza katika Operesheni hiyo Kaimu Meneja Kanda ya Magharibi (TBS), Rodney Alananga amesema wamefanya operesheni maalumu katika mkoa wa Katavi kwa bidhaa za Chakula na Vipodozi kwenye maghala, maduka makubwa ya jumla na rejareja, mipakani na bandarini kwa halmashauri nne ( Mlele, Mpimbwe, Tanganyika na Mpanda) na kubaini makosa kwa wafanyabiashara hao.
Amesema bidhaa ambazo zimeshikiliwa na shirika hilo zina thamani ya TZS 5,600,550/= hivyo basi TBS inatarajia kufanya uteketezaji wa bidhaa hizo baada ya taratibu zote za kisheria kufuatwa.
“TBS imechukua hatua za awali kwa kuzuia bidhaa zote zilizoonekana kuwa makosa ambazo utekelezaji na ufuatiliaji wake utaendelea ndani ya Siku 14 kwa mujibu wa notisi ya kuzuia bidhaa (seizure notice) mpaka 23/3/2022”. Amesema Alananga.
Katika Operesheni hiyo TBS Kanda ya Magharibi imeshirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo ofisi ya RPC,RAS, RSO, TRA, DC na kufanikisha zoezi hilo ambalo lilifanyika kuanzia Februari 21 hadi 27, 2022.