Breaking

Thursday, 17 March 2022

TANZANIA YAENDELEA KUWAWEZESHA WANAWAKE KUMILIKI NA KUSHIRIKI MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI

 

 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza katika mkutano wa pembeni kwa njia ya mtandao katika Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani.


Afisa kutoka Shirika la Landesa Tanzania Khadija Mrisho akichangia katika mkutano wa pembeni kwa njia ya mtandao jijini Dodoma katika Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani.



Baadhi ya Maafisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na wadau mbalimbali wakiwemo kutoka Shirika la Landesa Tanzania na Oxfarm wakiwa jijini Dodoma wakifuatilia mkutano wa pembeni kwa njia ya mtandao katika Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani.


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Amon Mpanju na Balozi wa Tanzania wa kudumu wa Umoja wa Mataifa New York Marekani Dkt. Kennedy Gastorn

************** 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Tanzania inaendelea kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi, kushiriki kwenye mipango ya matumizi ya ardhi iliyopo vijijini na utoaji wa maaamuzi katika changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.


Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo wakati akishiriki Mkutano wa pembeni ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani.


Dkt. Gwajima amesema kuwa Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mwanamke anapata fursa ya kumiliki ardhi hasa kwa wanawake wanaoishi vijijini kwani kumekuwa na changamoto katika kumiliki na kushirikishwa katika maamuzi ya matumizi ya ardhi hasa katika kilimo.


"Katika hili tumeweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha Mwanamke na Mtoto wa Kike wanawezeshwa kumiliki ardhi na kushiriki katika kuamua matumizi bora ya ardhi na kunufaika nayo" alisema Waziri Dkt. Gwajima


Waziri Dkt. Gwajima aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Amon Mpanju sambamba na baadhi ya Wataalam amesema, Mkutano wa Hali ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2022 unaongozwa na kauli mbiu ya "Kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na watoto wa kike kwa kupitia programu na sera yenye mtazamo wa mabadiliko ya tabia nchi na mazingira na upunguzaji wa athari za majanga"


Wakati huo huo wataalam wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Idara ya Maendeleo ya Jinsia kwa kushirikiana na wadau wameshiriki Mkutano huo kwa njia ya Mtandao wakiwa  Jijini Dodoma ikiwa ni kuupa nguvu Mkutano unaoendelea nchini Marekani na kutia msukumo ajenda iliyojadiliwa katika mkutano huo.


Akizungumza baada ya Mkutano huo, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Idara ya Maendeleo ya Jinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Rennie Gondwe amesema lengo la Mkutano huo wa pembeni ndani ya Mkutano wa 66 wa hali ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii na kuwa na usawa na haki katika kumiliki na kutumia ardhi na kutoa maamuzi.


Rennie ameongeza kuwa, Wizara kwa kushirikiana na wadau inatekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wenye maeneo manane ikiwemo eneo la Mila na Desturi ambapo unasaidia pia kutoa hamasa kwa jamii na wadau kutoa elimu ya kumuwezesha Mtoto wa kike na Mwanamke kumiliki na kunufaika na ardhi.


Akichangia kwenye Mkutano huo Mkurugenzi wa Landesa Tanzania Dkt. Monica Mhoja, amesema Shirika lake linashirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha mwanamke haachwi nyuma kunapo umiliki wa ardhi na kupata manufaa  hasa katika uzalishaji na matumizi bora ya ardhi.


Ameongeza kuwa lengo la Shirika hilo ni kuangalia ni kwa namna gani makundi hasa ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanashirikishwa kwenye mpango wa matumizi ya ardhi hususan katika ngazi ya kaya ili ardhi hiyo iweze kuwanufaisha katika ustawi wao.


MWISHO

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages