Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi makubwa ya ugonjwa wa kifua kikuu ambazo zinachangia asilimia 87 ya wagonjwa wote duniani.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu leo Alhamisi Machi 24, 2022 kwenye maadhimisho siku ya kifua kikuu ambapo kitaifa yamefanyika mkoani Tanga.
Waziri Ummy amesema kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2021 inasema kulikuwa na wagonjwa wapya wa kifua kikuu milioni 9.9 duniani kote na kati ya hao wagonjwa milioni 1.4 sawa na asilimia 14 walifariki.
"Mwaka huo Tanzania ilikua na wagonjwa wapya wa kifua kikuu 133,000 sawa na wagonjwa 222 kwa kila watu 100,000 ikionesha maambukizi kupungua kwa asilimia 27 ukilinganisha na miaka mitano iliopita". Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi za kuweza kuwafikia na kuwaweka katika matibabu wenye uhitaji wa huduma ya matibabu ya TB hadi kufikia asilimia 64.
"Kila mmoja wetu anawajibu wa kujitolea kwa hali na mali ili kuweza kuwafikia wagonjwa wapatikane ili wapate matibabu na kuyafikia malengo yetu ya kuudhibiti ugonjwa huu". Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ambaye hajagundulika na kuwekwa katika matibabu ana uwezo wa kuambukiza watu kati ya 10 mpaka 20 kwa mwaka.
Katika kuendeleza juhudi za kudhibiti ugonjwa huu Serikali imeboresha huduma za uchunguzi na uuguzi kwa kuwekeza katika teknolojia ya kisasa pamoja na kusambaza magari 11, mashine za Gene Xpert 50, Mashine za ECG 179 na pikipiki 179 zenye thamani ya Tsh: Bilioni 6.8.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema nchi yetu ipo katika mapambano ya Magonjwa ya mlipuko wa mfumo wa hewa ambayo mengine yanashabihiana na kifua kikuu pamoja na UVIKO-19.
"Nitoa rai kwa wananchi wote tunapoadhimisha siku hii ya kifua kikuu duniani, tuendelee kujikinga na Magonjwa haya kwa kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu." Amesema Waziri Ummy