Breaking

Saturday, 26 March 2022

SERIKALI YAWEKA MAPINGAMIZI MANNE KESI YA MAKONDA

 


Jamhuri imeweka mapingamizi katika maombi yaliyofunguliwa na Mwanahabari nchini humo, Saed Kubenea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, kuomba kibali cha kumfungulia kesi ya matumizi mabaya ya madaraka, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. 


Mapimizi hayo yaliyowekwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), yametajwa Machi 25, 2022 na Wakili wa Kubenea, Hekima Mwasipu, wakati maombi hayo yalipokwenda kutajwa mahakamani hapo.


Wakili Mwasipu ameyataja mapingamizi hayo yaliyodai kuwa, Kubenea hana maslahi na maombi hayo, mahakama hiyo haina mamlaka ya kuyasikiliza, sheria iliyotumika kuyafungua kutokuwa na nguvu, pamoja na maombi hayo kutokana na habari za kusikika.


“Mapingamizi yako manne, pingamizi la kwanza linasema Kubenea hana maslahi na hii kesi. Pili, wanasema mhakama hii haina mamlaka ya kuyasikiliza,” amesema Wakili Mwasipu


“Tatu wanasema wakati tukio linatokea (Makonda kuvamia Ofisi za Kampuni ya Clouds Media), tarehe 17 Machi 2017, sheria ambayo tumetumia kuleta maombi ilikuwa haina nguvu kwa wakati huo na la mwisho wamesema maombi yote yaliyoletwa katika mahakama hii, yametokana na habari za kusikika.”


Hekima Mwasipu ameyataja mapingamizi hayo, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Subira Mwalumuli, kutotaja hadharani hoja za mapingamizi hayo.


Mnamo tarehe 2 Machi 2022, Wakili Mwalumuli aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Aron Lyamuya, kwamba DPP na DCI, wanakusudia kuleta mapingamizi ya awali.


Awali, Wakili wa Kubenea, Nyaronyo Kicheere, aliiomba mahakama hiyo iahirishe maombi hayo hadi siku nyingine, kwa ajili ya kupanga tarehe ya kusikiliza mapingamizi ya wajibu maombi.


Kicheere alitoa maombi hayo baada ya Wakili wa Makonda, Goodchance Reginald, kuchelewa kuwasilisha hati kinzani kwa upande wa waleta maombi.


Baada ya mawakili wa pande zote mbili kukubali hoja ya ahirisho hilo, Hakimu Lyamuya aliahirisha maombi hayo hadi tarehe 29 Aprili 2022, kwa ajili ya kuja kutaja tarehe ya utoaji maamuzi ya mapingamizi ya Jamhuri.


Hakimu Lyamuya alitoa siku 14 kwa upande wa Jamhuri, kuwasilisha hoja za mapingamizi kwa njia ya maandishi, tarehe 8 Aprili 2022. Kisha upande wa waleta maombi kuwasilisha majibu ya mapingamizi hayo kwa maandishi tarehe 22 Aprili mwaka huu.


Katika maombi hayo, Kubenea anamtuhumu Makonda kwa matumizi mabaya ya ofisi, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ikidai alivamia Ofisi za Kampuni ya Clouds Media Group, jijini Dar es Salaam, tarehe 17 Machi 2017.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages