Breaking

Saturday 19 March 2022

SERIKALI YATENGA BILIONI 1 MAFUNZO YA WANAWAKE WAONGOZA WATALII NCHINI



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mpango wa  Maendeleo na Ustawi wa Taifa  wa Mapambano dhidi ya UVIKO -19 imetenga shilingi bilioni 1.01 kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo waongoza watalii wanawake takribani 1060 nchini.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mary Masanja  wakati wa kuhitimisha mafunzo ya waongoza Watalii wanawake 89 yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.



“Mafunzo haya ni mahususi kwa wanawake kama jitihada za makusudi kabisa za Serikali kuhakikisha kuwa wanawake wanapata fursa za kuchangia katika maendeleo ya nchi kupitia utalii na kunufaika kupitia sekta hiyo” ” amefafanua Mhe. Masanja.


Amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri kwa kuitangaza vyema Tanzania ndani na nje ya nchi.


 “Natambua mmekuwa mabalozi muhimu mnaotegemewa kuiuza nchi yetu hivyo sifa ya kwanza mnayotakiwa kuwa nayo ni uzalendo. Wageni mnaowapokea wana sifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa hivyo wakati mnatekeleza majukumu yenu mnapaswa kuwa na uelewa mpana wa shughuli za utalii na pia muwe na maadili, weledi na uadilifu”amesema Mhe. Masanja.



Aidha, amewaasa waongoza watalii hao kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa watalii wanapowasili nchini ili kujenga taswira nzuri ya Tanzania na kumfanya mtalii aweze kurudi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages