Breaking

Friday, 25 March 2022

SEKTA YA SANAA NA BURUDANI IKISIMAMIWA VIZURI ITALETA MANUFAA MAKUBWA - WAZIRI MCHENGERWA



Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa  amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazotoa mchango mkubwa wa fedha katika taifa kutokana na sekta za burudani.


Waziri Mchengerwa ameyasema haya Alhamisi Machi 24, 2022 wakati alipokuwa akiwasilisha  maelezo ya rasimu  ya mpango wa bajeti ya Wizara  kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa  Kamati ya  Kudumu ya Bunge  ya  Huduma  na Maendeleo ya Jamii katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.  


Amesema  tafiti zilizofanywa na kampuni ya PricewaterhouseCoopers (PWC) katika nchi za Afrika, sekta za burudani na vyombo vya mawasiliano (Entertainment and Media (E&M), An African perspective) katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2022 zinaonyesha kuwa sekta hizo  zinatoa mchango mkubwa wa kifedha katika nchi hizo. 


 “Katika kipindi cha mwaka 2017 mapato ya ujumla kutokana na sekta za burudani na vyombo vya mawasiliano (Entertainment and Media – E&M) katika Tanzania yalifikia Dola za Marekani milioni 496 (sawa na shilingi Trilioni 1.17) ambapo yaliongezeka kwa asilimia 28.2 kutoka mwaka 2016. Kwa kuendelea ukuaji wa wastani wa asilimia 18.3 mapato hayo yanatarajiwa kufikia Dola bilioni 1.1 (sawa na shilingi Trilioni 2.59) mwaka 2022”. Amefafanua Waziri Mchengerwa.


Amesema mwaka 2018 sekta za burudani hapa nchini ilikuwa kwa asilimia 13.7 na kuongoza kwa ukuaji ambapo ilifuatiwa na sekta ya ujenzi. Mwaka 2019 ilishika nafasi ya pili kwa kukua kwa asilimia 11.2.


Ameongeza kuwa sekta ya sanaa na burudani ikisimamiwa vizuri inamchango mkubwa kwa mawanda ya ajira, kuchangia uchumi pamoja na kukuza na kuendeleza utalii. 


 "Kwa ujumla Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo zina umuhimu mkubwa sana katika maendeleo ya nchi kwa upana wake na kwa mwananchi mmoja mmoja. Pamoja na mambo mengine, Sekta hizi zina nguvu kubwa ya ushawishi, uhamasishaji na ustawishaji wa jamii na maendeleo ya nchi. Kutokana na msingi na umuhimu wake huo, Sekta hizi zinafahamika kama Nguvu Laini (Soft Power) ya Nchi”. Amesisitiza Mhe. Mchengerwa.



Pia amesema kwa umuhimu wake, sekta hizi zimekuwa na mvuto mkubwa kwa makundi mabalimbali ya jamii na hususan vijana ambao ndio wanaunda sehemu kubwa ya nguvu kazi ya nchi, ambapo amefafanua kwamba kwa kuzingatia hali hiyo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) 2021/22 – 2025/26s navyo vimeelezea umuhimu wa Sekta hizi katika kuleta maendeleo makubwa ya nchi.


Akizungumzia kuhusu utoaji wa tozo za muziki, Waziri Mchengerwa amesema wizara imesikia maoni ya wadau na inakwenda kufanya  mapitio ya kanuni na taratibu ya utoaji wa tuzo kabla tukio la utoaji wa tuzo hizo ili wasanii waweze kupata haki zao.



Mwenyekiti Kamati hiyo Stanslaus Nyongo amemshukuru Waziri kwa ubunifu mkubwa ambapo amesema anaimani kuwa anakwenda kuleta mapinduzi makubwa ambapo ameishauri Wizara  kushirikisha wadau wa sekta binafsi kwenye  kuwekeza kwenye michezo.


Ameitaka Wizara kuwa na program maalum ya kuhamasisha  ufanyaji wa mazoezi ili kusaidia kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza.


Aidha aimeitaka Wizara kukaa jirani na wadau wa sekta hizo na kuwasilikiza ili waweze kufanya vizuri zaidi katika kukuza na kuendeleza sekta hizo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages