Breaking

Saturday, 26 March 2022

SAMIA CUP - MTAA KWA MTAA YAIVA

 



Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema mwongozo wa program ya michezo na sanaa ya mtaa kwa mtaa imekamilika na utawasilishwa kwenye kikao kazi cha maafisa utamaduni na michezo kinakachofanyika mwanzoni mwa mwezi Aprili 2022 jijini Dodoma. 


Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Machi 26,2022 mara baada ya  ziara yake ya kikazi aliyoambatana na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dkt. Hassan Abbasi kukagua miundombinu mbalimbali ya uwanja wa Benjamini Mkapa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa chumba maalum cha mazoezi ya viongo (Gym) baada ya kupata wasilisho kuhusu program mtaa kwa mtaa  kutoka Idara ya Maendeleo ya Michezo na Baraza la Michezo (BMT) nchini.


Waziri Mchengerwa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeamua kuratibu na kuendesha mashindano ya michezo ya kitaifa  yatakayojumuisha  michezo mbalimbali ambayo yataanzia  katika ngazi ya mtaa na kujulikana  kwa jina la SAMIA CUP -Mtaa kwa Mtaa kisha kwenda kitaifa ambapo yataitwa SAMIA TAIFA CUP.


Waziri Mchengerwa ameongeza” katika michezo”mtaa” umepewa maana mbalimbali  ili  viongozi wa Serikali waweze kusimamia, kutembelea na kuweka  mageuzi stahiki kwa maendeleo ya Sanaa nzima”


Mhe. Mchengerwa ameeleza malengo ya program hii kuwa ni pamoja na kuibua vipaji vya michezo na Sanaa katika ngazi ya mitaa, vijiji, kata, tarafa, Wilaya na Mikoa na hatimaye Taifa,kuunganisha na kujenga mshikamano katika jamii pamoja na  ujenzi wa uchumi binafsi na nchi kwa ujumla pamoja na  kutoa fursa kwa wananchi kwa ngazi zote za Serikali kushiriki kwa vitendo shughuli za Michezo na Sanaa ili kunufaika na faida zake.


Amesisitiza kuwa mkakati wa michezo mtaa kwa mtaa ni mpango mpya uliobuniwa na Wizara ili kuhakikisha kuwa wananchi hususan vijana wanapatiwa fursa kubwa ya kuoonesha vipaji vyao katika ngazi zote.


 Ameitaja michezo itakayohusishwa katika program hii kuwa ni pamoja na riadha, mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mchezo wa netiboli, mpira wa wavu, michezo ya jadi na sanaa za ndani.


 Amesema matokeo tarajiwa katika program hii ni vijana zaidi ya 80,000 kuweza kushiriki katika ngazi ya kata hadi mkoa, vijana kutoka ngazi za vijiji na mtaa kuweza kupata nafasi ya kuonekana kwenye ngazi ya taifa na vijana wenye vipaji kupata nafasi ya kujiunga na maalum za michezo (academies).


Akitoa wasilisho hilo Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusufu Singo amefafanua dhana ya mtaa kwa mtaa katika maana tatu ambapo amesema maana ya kwanza ni mtaa ikiwa  na maana ya mtaa wa sasa wa Serikali ambapo amesema  hadi  sasa  mitaa inafika takribani 400 nchi nzima.



Aidha, Singo amesema  maana ya pili ya mtaa inajumuisha shule, vyuo na taasisi ambapo amesema  hii itajumuisha mashindano kama ndondo CUP, mashindano ya vijana ya TFF, Coca Cola, Umitashumta, umiseta na mashindano ya taasisi kama SHIMIWI,SHIMUTA NA SHIMISEVITA.Amesema maana ya mwisho ya mtaa ni ligi mbalimbali za kitaifa za michezo.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages