Na Samir Salum - Lango la habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuruhusu wananchi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba kwa utaratibu wa mpangaji au mnunuzi.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo Jumatano Machi 23, 2022 wakati akızindua nyumba 644 za makazi za Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam ambazo ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 52.
Rais samia amesema kuwa wakazi hao ambao wameahidiwa kukaa bure kwa miaka mitano ameridhia walipie gharama za ujenzi wa nyumba pekee bila ya gharama za ardhi na miundombinu ya jumuiya baada ya miaka hiyo.
"Nimeridhia kuwa baada ya miaka mitano wananchi wa Magomeni Kota kuuziwa nyumba kwa utaratibu wa mpangaji au mnunuzi na kurejesha gharama za ujenzi wa nyumba pekee, hatutawatoza gharama ya ardhi kwa sababu tukifanya hivyo mtashindwa kuzinunua" amesema Rais Samia
Ameongeza kuwa wale wanaotaka kulipa gharama ya ununuzi kabla ya kufika miaka mitano wanaruhusiwa kulipa kidogo kidogo kwa kipindi cha miaka bila ya riba yoyote.
Rais Samia amewaasa wakazi hao kutunza nyumba hizo na kuzingatia usafi wa ndani na nje na kuchangia huduma jumuishi kwa faida ya kila mmoja.
"Nawaomba matunzo katika nyumba hizi ikiwemo usafi, usafi wa nyumba dhamana iko kwenu. Nyumba kama hizi tunategemea watu mpikie gesi na hatutegemei mtatumia kuni" Amesisitiza Rais Samia
Aidha, Rais Samia amewataka TBA, NHC na Watumishi Housing kukaa na sekta binafsi ili kukubaliana katika ujenzi wa makazi bora kwenye maeneo yanayopaswa kuendelezwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amesema Makalla amesema ujio wa Rais Samia umemaliza mambo mawili ikiwemo kufuta fitina zote zilizokuwa zikijengwa juu ya wakazi wa Magomeni Kota na kuwa ndio mwisho wa matapeli maana kuna watu walikuwa wanawaonesha watu nyumba hizo na kuwaambia zinapangishwa.
Imeelezwa kuwa mahitaji ya nyumba bora yanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni 3 nchi nzima, huku ongezeko la mahitaji ya nyumba bora ni takribani laki mbili kila mwaka.