ZAIDI ya shilingi Bilioni 234 zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuimarisha Sekta yta Afya nchini.
Hayo yamesemwa leo Machi 1, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia madarakani.
"Katika Sekta ya Afya fedha tumepokea kwa kipindi cha miezi 11 ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan madarakani Shilingi bilioni 234.41 ambazo zimetumika katika ujenzi wa vituo vya afya 288, hospitali mpya 28,majengo ya wagonjwa mahututi 26.
"Pia kuna ujenzi wa majengo ya dharura 80 (Emergency Medical Department- EMD), ujenzi wa kituo kimoja cha Matibabu ya Magonjwa ya Milipuko, nyumba 150 za watumishi za 3/1 katika maeneo ya pembezoni, ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati 615.
"Utekelezaji mwingine ni ukamilishaji wa ujenzi wa hospitali 68 za halmashauri zilizoanza kujengwa mwaka wa fedha 2018/19, uendelezaji ujenzi wa hospitali 31 za halmashauri na ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa hospitali 31,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Bashungwa.
Ameongeza kuwa, katika Sekta ya Afya fedha ambazo zinatarajiwa kupokelewa kwa kipindi cha kuanzia Machi hadi Juni, 2022 ni shilingi bilioni 263.72 ambazo zitatumika kujenga vituo vya afya 288 zikiwemo hospitali mpya 28.
Pia amesema, fedha hizo zitatumika kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati 167,ukamilishaji wa ujenzi wa hospitali 68 za halmashauri zilizoanza kujengwa mwaka wa fedha 2018/19.
Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema kuwa, fedha hizo zitatumika kuendeleza ujenzi wa hospitali 31 za halmashauri, ununuzi wa vifaa vya huduma za wagonjwa mahututi na amgari 195 ya kubeba wagonjwa.
"Vile vile zitatumika kununulia vifaa vya Idara ya Dharura 80, mfumo wa usambazaji hewa tiba ya Oksijeni,mashine ya Kidigiti ya Mionzi, magari 212 ya usambazaji na usimamizi, kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi, ajira za watumishi za muda kwa miezi sita na ununuzi wa vifaa na tiba kwa hospitali,"ameeleza Waziri Bashungwa.