Meli ya mizigo iliyokuwa imebeba maelfu ya magari ya kifahari imezama katika visiwa vya Ureno vya Azores, karibu wiki mbili baada ya kushika moto.
Meli hiyo inayoitwa Felicity Ace, ilikuwa ikisafirisha magari ya kifahari 4,000 yakiwemo aina ya Porsches na Bentleys.
Meli hiyo ilikuwa njiani kuelekea Rhode Island nchini Marekani kutoka bandari ya Ujerumani ya Emden wakati moto ulipozuka Februari 16, 2022 ambapo Wahudumu wote wa meli hiyo waliokolewa.
Joao Mendes Cabecas, nahodha wa moja ya bandari iliyo karibu katika kisiwa cha Faial, amesema kuwa hakuna uvujaji wa mafuta ulioripotiwa hadi sasa lakini alisema kuna hofu kwamba matenki ya mafuta yanaweza kuharibika wakati chombo hicho kikiwa chini ya bahari ya Atlantic katika kina cha mita 3,500 (maili 2.17).
Jeshi la wanamaji la Ureno limesema hakuna aliyejeruhiwa na moto huo na kwamba wafanyakazi wote 22 wa meli hiyo walipelekwa katika hoteli moja baada ya jeshi la wanamaji, meli nne za wafanyabiashara waliokuwa wakisafiri katika eneo hilo na Jeshi la Anga la Ureno kukamilisha zoezi hilo la kuwokoa.
Volkswagen imesema uharibifu wa magari hayo yenye bima unaweza kugharimu karibu $155m kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Bentley alithibitisha kuwa magari yake 189 yalikuwa ndani ya meli hiyo na kampuni ya Porsche ilisema ilikuwa na magari 1,100 katika meli hiyo.