Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC), imeridhishwa na namna uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ulivyosimamia miradi ya maendeleo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Zedi ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 18, 2022 katika ziara ya kamati ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Manispaa hiyo waliombatana pia na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange.
Katika ziara hiyo, Kamati imepokea taarifa ya mradi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) la Hospitali ya Wilaya ya Kahama ambalo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 97 na unajengwa kwa mapato ya ndani ya Manispaa hiyo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Zedi ameshauri uongozi huo kusimamia ujenzi wa jengo la OPD ukamilike kwa haraka ili wananchi wapate huduma.
Awali, akitoa maelezo ya ujenzi huo, Dkt. Lucas Ngamtwa amesema jengo hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa wasiopungua 1,000 na ujenzi wake umezingatia uwekwaji wa mifumo ya mashine za kieletroniki.
Katika hatua nyingine, Kamati imekagua mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Manispaa hiyo katika Kata ya Kahama mjini eneo la wafanya biashara wadogo wadogo na kuridhishwa na kikundi cha SACOSS CDT kilichopatiwa sh. milioni 100 kilivyojiendeleza biashara ndogo ndogo za mamalishe, wauza matunda.
Kikundi hicho kimezingatia uwapo wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Akisoma taarifa ya kikundi, Mwenyekiti wa kikundi cha CDT, Charles Wilson amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutilia mkazo na kuweka Sheria ya kutenga fedha hizo kwa makundi hayo.
Aidha, ameomba Sheria iwapunguzie kundi la watu wenye ulemavu marejesho yao yawe ni tofauti na wengine.
Hata hivyo, Kamati imeushauri uongozi wa Manispaa hiyo kusimamia
urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa ili vikundi vingine vikopeshwe.