Breaking

Saturday, 19 March 2022

KINYESI CHA MIFUGO CHANZO CHA KUFA SAMAKI MTO MARA - KAMATI



Kamati maalum ya kitaifa iliyoundwa na serikali kuchunguza mabadiliko ya maji ndani ya mto Mara, imetoa taarifa ya chanzo cha mabadiliko katika mto huo yaliyosababisha maji kuwa meusi na kutoa harufu, huku samaki wakifa ambapo chanzo kimeelezwa kuwa ni shughuli za binadamu pamoja na nguvu za asili.

Akitoa matokeo ya uchunguzi leo Jumamosi Machi 19, 2022 mjini Musoma, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Samuel Manyele amesema kuwa hali hiyo imetokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha kinyesi cha mifugo mtoni pamoja na uozo wa mimea ndani ya mto hasa mimea vamizi kama vile magugu maji na matete.

Professa Manyele amesema kuwa hali hiyo ilisababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kiwango cha oksijeni ndani ya mto na hivyo maji kubadilika rangi na kuwa na harufu mbaya huku samaki wakikosa chakula na hivyo kusababisha vifo vyao.

SomaWAZIRI JAFO ATEUA KAMATI YA UCHUNGUZI WA UCHAFUZI WA MAZINGIRA MTO MARA


Amesema kuwa kwa mujibu wa uchunguzi waliofanyana walibaini kuwa mabadiliko hayo ni matokeo ya mvua kubwa iliyonyesha ghafla kwa muda mfupi katika kipindi cha mwezi huu hivyo kutibua uchafu uliokuwa umejikusanya chini ya mto kwa muda mrefu.

"Mvua zingeendelea kunyesha hali hii ingeisha kwani uchafu ungetiririshwa lakini kwa vile mvua zimenyesha na kukatika ghafla ina maana uchafu ule unatoka taratibu na hii hali inaweza kudumu kwa zaidi ya miezi mitatu hadi minne endapo mvua hazitanyesha hapa katikakati," amesema.

Profesa Manyele amesema kuwa mto huo umeathiriwa kuanzia katika kijiji cha Marasibora wilayani Rorya na kijiji cha Wegero wilayani Butiama huku akisema kuwa mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara hauhusiki na uchafuzi huo.

"Mgodi upo mbali sana na maeneo yaliyoathirika na hata kama uchafu unaozalishwa mgodini pale ungezidishwa mara ishirini na kumwagwa mtoni maji yasingebadilika rangi wala kuwa katika hali iivyo sasa na maji ya mto kelekea kule mgodini ni masafi na hayana shida yoyote," amesema.

Amesema kuwa wamebaini uwepo wa kinyesi cha ng'ombe zaidi ya tani 1.8 milioni pamoja na mkojo wa ng'ombe lita 1.5 bilioni uchafu uliotokana na kuwepo kwa ng'ombe zaidi ya laki 3 waliokuwepo katika eneo oevu la mto Mara kwa kipindi cha miezi minane mwaka jana wakati wa kiangazi.

"Ng'ombe mmoja ana toa kilo 25 za kinyesi kwa siku moja na mkojo lita 21 kwa siku kwahiyo ukizidisha kwa idadi hiyo ya ng'ombe mara miezi minane utapata kiwango hicho na hapo bado hatujaweka kinyesi na mkojo wa kondoo, mbuzi na punda," amesema.

Soma : WAZIRI JAFO ATEUA KAMATI YA UCHUNGUZI WA UCHAFUZI WA MAZINGIRA MTO MARA


Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jafo ametoa muda wa siku mbili kwa kamati hiyo kuandaa taarifa kamili yenye mpango kazi juu ya nini kifanyike na muhusika ni nani kisha taarifa hiyo ikabidhiwe kwake kwaajili ya utekelezaji.

Soma : WAZIRI JAFO ATOA UFAFANUZI WA RIPOTI YA MTO MARA, AWATAKA WATANZANIA KUWA WATULIVU

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages