Breaking

Monday, 21 March 2022

KIKOSI KAZI CHABAINI TUME YA UCHAGUZI SIO HURU, CHAPENDEKEZA MCHAKATO WA KATIBA MPYA KUANZA 2025



Mwenyekiti wa Kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini profesa 
Rwekaza Mukandala, amesema kuwa tume zote mbili za uchaguzi siyo huru na kwamba wapo baadhi ya watendaji katika tume hizo ambao wanavunja sheria za uchaguzi.


Profesa Mukandala ameyasema hayo hii leo jumatatu Machi 21, 2022 wakati kikosi kazi kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi ilipokutana na Rais Samia Suluhu Hassan ili kumkabidhi taarifa ya kikosi kazi hicho. 

Profesa Mukandala amesema kuwa  wamebaini kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa unakuwa mgumu kwasababu unasimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI jambo linalowapelekea baadhi ya wananchi walioandikishwa kupiga kura kutoshiriki kikamilifu na hata kutokupiga kura kabisa, na kwamba kuna haja ya kufanyia marekebisho sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa.

Kikosi kazi hicho pia kimependekeza kwamba kuna ulazima wa Tume Ya Uchaguzi kufanyiwa tathimini, lakini pia ufanyike ubainifu kisha mapendekezo ya namna bora ya kuwa na Tume Huru Ya Uchaguzi katika nchi yetu.

Profesa Mukandala amesema kuwa kikosi kazi hicho kimebaini kuwa mchakato wa katiba mpya uliacha baadhi ya mambo ya msingi katika Katiba pendekezwa. 

Kikosi kazi kilichoteuliwa na msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kimependekeza mchakato wa kupata Katiba Mpya uanze baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Samia 
amekitaka Kikosi Kazi hicho kuja na mapendekezo ya mchakatako wa Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na kukomesha rushwa.

“Hili la Katiba mpya mtakwenda kulifanyia kazi na mtaleta mapendekezo yatakayotangazwa Watanzania wote wayaelewe, Mimi nakubaliana kuwa ni jambo la muda mrefu lakini Watanzania wote waelewe" amesema Rais Samia na kuongeza:

“Lakini kwanza tukayafanyie kazi haya marekebisho tuliyoyasema haya kipindi hichi cha muda wa kati halafu huko mbele tuone je tuna haja ya kurekebisha katiba yetu pengine kutakuwa na haja sio ya kuandika mpya, kurekebisha baadhi ya maeneo na hata kama tunaandika mpya lakini kazi kubwa inakuwa imefanyika kwenye marekebisho ambayo tunakuwa tumeyafanya kule ni kwenda kuingiza tuu kwenye hiyo katiba.”

Kwa upande mwingine Rais Samia amesema Kikosi Kazi hicho pia kinatakiwa kushughulikia masuala ya rushwa kwenye jamii, Uchaguzi pamoja na masuala mbalimbali ya siasa.

''PCCB haifanyi kazi yake ipasavyo, hili sio la uongo ni kweli ingawa ukisema wenyewe wanakasirika. Ukisema Jeshi la Polisi halifanyi kazi vizuri unakwenda kujibiwa... hatufanyi kazi vizuri, hauamini vyombo vyako?'' - ameeleza Rais Samia.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages