Breaking

Saturday, 26 March 2022

TOPE LA UOZO WA MAGUGU CHANZO CHA UCHAFUZI WA MAJI MTO MARA : KAMATI

Komando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania Sajenti Cosmas Aloyce Nyakaho akichukua sampuli ya Maji kwenye mto Mara ikiwa ni sehemu ya kuchunguza sababu za kuchafuka kwa Mto huo hivi karibuni


Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kuchuguza chanzo cha kuchafuka kwa Mto Mara Prof. Samweli Manyele amesema kufuatia uchunguzi wa kimaabara uliofanyika kwenye sampuli zilizochukuliwa katika maji ya Mto Mara hivi karibuni imebainika kuwa chanzo kikuu cha kuchafuka kwa Mto Mara ni kusambaa kwa tope la uozo wa viumbe-vifu lililotibuliwa na mvua kubwa ilionyesha kwa kipindi cha muda mfupi.

Prof. Manyele amesema hayo leo tarehe 26.03.2022 alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya uchunguzi wa kuchafuka kwa Mto Mara.

Amesema kuwa sababu kubwa ya kuchafuka kwa Mto Mara imetokana na mrundikano wa kiwango kikubwa cha tope lililosababishwa na uozo wa viumbe (organic matter) kilichobainika chini ya ardhi oevu ya huo.

Amevitaja viumbe hivyo ni pamoja na mimea ya matete, magugu maji na uwepo wa vinyesi vya wanyama uliosababishwa na wingi wa mifugo iliyopo katika eneo hilo.


Vilevile, Kamati yake imebaini kukosekana kwa hewa ya Oxygen katika maji ya Mto Mara hali iliyopelekea vifo vya Samaki nakusema kuwa hali hiyo imetokana na mmeng’enyo wa viumbe-vifu wakati wa uozeshwaji wake chini ya maji uliosababishwa na wingi wa mimea maji kwenye eneo oevu la Mto Mara.

Soma : WAZIRI JAFO ATOA UFAFANUZI WA RIPOTI YA MTO MARA, AWATAKA WATANZANIA KUWA WATULIVU

Katika taarifa yake Prof. Manyele amesema vipimo vya awali vya ubora wa maji vilionyesha uwepo wa mafuta hali iliyolazimu kufanyika kwa utafiti wa kina na matokeo ya sampuli yalionesha kuwa utando wa mafuta unaonekana juu ya maji ya Mto Mara unatokana na mchakato wa uozaji wa viumbe-vifu vya mimea vilivyopo kwenye eneo oevu la Mto Mara.



Kufuatia kukamilika kwa taarifa ya kina ya uchunguzi wa kuchafuka kwa Mto Mara, Kamati ya Kitaifa imeshauri maji ya Mto huo yanaweza kutumika kwenye shughuli mbalimbali za binadamu kwa kuwa sampuli zilizochukuliwa na kufanyiwa vipimo hazikuonesha kuwepo kwa kemikali za sumu na kusema kuwa viumbe kama Samaki ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Pia Soma KINYESI CHA MIFUGO CHANZO CHA KUFA SAMAKI MTO MARA - KAMATI

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages