Breaking

Friday 18 March 2022

JESHI LA POLISI LATAKIWA KUWACHUKULIA HATUA ASKARI WANAOJIHUSISHA NA UHALIFU

 



Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini ameuagiza Uongozi wa Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kuzuia uhalifu na kuwashughulikia wahalifu wote watakaobainika hata kama ni maofisa, wakaguzi au askari wa Jeshi la Polisi.

Ameyasema hayo Machi 17, 2022 katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi, Kambi ya Kambapori iliyopo Mkoani Kilimanjaro wakati akifunga mafunzo ya uongozi mdogo wa cheo cha Koplo wa Polisi katika Shule ya Polisi iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo jumla ya askari 1751 wamehitimu mafunzo hayo.

Naibu waziri Sagini amesema kuwa anachukizwa na askari wanaoshiriki katika matukio ya kihalifu hali inayowafanya wananchi kutokuwa na imani na jeshi hilo.



Ameliagiza Jeshi la polisi kuchukua hatua za kuzuia uhalifu na kuwashughulikia wahalifu wote watakaobainika hata kama ni maofisa, wakaguzi au askari wa Jeshi la Polisi.

Amewataka askari Polisi kote nchini kuendelea kutumia weledi,maadili na ushirikishwaji wa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Ninawaasa askari wa Polisi mtakapotoka hapa, mwende mkafanye kazi kama mlivyofundishwa, msifanye kazi kama mlivyozoea. Hakikisheni mnafanya kazi zenu kwa kufuata Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali iliyopo na itakayokuwa ikitolewa na viongozi wenu.”


Aidha, Naibu Waziri Jumanne Sagini amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kuruhusu kupandishwa vyeo kwa maafisa, wakaguzi na askari wangazi mbalimbali wa vyombo vyotevilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Akizungumza na wahitimu Naibu Waziri Sagini kuwaagiza askari hao kwenda kuyashughulikia makosa ya uhalifu wa kimtandao ambapo baadhi yamekuwa yakidhalilisha utu, kuchochea chuki na uhasama katika Jamii zetu pamoja na kuathiri uchumi na kutishia amani, utulivu na usalama
.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages