Nondo ambaye ni mwenyekiti wa Ngome ya vijana wa chama cha ACT Wazalendo alikuwa anashtakiwa kwa makosa mawili, moja ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni na mbili, kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga.
Awali, Nondo aliachiwa huru na Mahakama Kuu ya Tanzania baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha makosa yaliyokuwa yanamkabili bila kuacha shaka yoyote.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliokuwa umempa ushindi Nondo.
Leo Jumatano Machi 23, 2022, kesi ilikuwa inafika mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa lakini Wakili wa Serikali, Basilius Namkambe aliwasilisha ombi mahakamani kuwa DPP hana nia ya kuendelea nayo.
Kesi hiyo iliyokuwa chini ya majaji watatu, Shaban Ally Lila, Ignas Paul Kitusi na Abrahamu Mwampash na imeondolewa chini ya kanuni namba 77, kanuni ndogo ya nne za kanuni za Mahakama ya Rufaa.
Kwa upande wake Abdul Nondo amesema kuwa anamshukuru Mungu kwani yupo huru na ataendelea na kazi zake kama kawaida.
“Hii kesi haikuwa na ushahidi wowote, nashukuru Mungu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu iliona hakuna ushahidi wowote. Nashukuru leo kesi imeondolewa kwa hiyo nipo huru,” amesema Nondo.
Wakili wa kujitegemea aliyekuwa anamtetea Nondo, Jebra Kambole amesema wanashukuru kuwa upande wa Serikali imeona haina nia ya kuendelea na kesi hiyo iliyokaa muda mrefu.