Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bi. Jasinta Mboneko ametoa Zawadi ya viti na meza kwa shule za sekondari Ibinzamata na Ndala zilizipo katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga pamoja na Shingita iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa kufanikiwa kuondoa daraja sifuri katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne uliofanyika mwezi Novemba 2021.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuzipongeza Shule hizo iliyofanyika leo Ijumaa Machi 04, 2022 katika shule ya Sekondari Ibinzamata, Dc Mboneko amewataka walimu, wazazi na wadau mbalimbali wa elimu kuendelea kushirikiana kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaoandikishwa shuleni wanafaulu na kuendelea na masomo ya ngazi za juu.
"Mwaka jana nilifanya ziara katika shule zote za sekondari zilizopo katika Manispaa ya Shinyanga na nikawaelekeza walimu kuwa moja ya malengo yetu kama Wilaya katika elimu ni kuondoa daraja sifuri. Nashukuru Shule za Sekondari Ibinzamata, Ndala na Shigita zimefanikiwa kufikia malengo tuliyojiwekea" Amesema Dc Mboneko
Aidha, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanawachangia watoto wao chakula cha mchana shuleni hali itakosaidia kuongeza ufaulu.
" Tusidanganyane hapa, hakuna mtu ambaye anaweza kusoma vizuri huku akiwa na njaa. Kinachofanyika ni kubadilisha tu kile chakula alichopaswa mtoto kula nyumbani wakati wa mchana kama kweli tunayo nia ya dhati na tunataka watoto wetu wafaulu vizuri basi hatuna budi kuhakikisha kuwa wanapata chakula wakiwa shuleni." Amesisitiza Dc Mboneko.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Ibinzamata, Ezekiel Sabo, akitoa neno la shukrani kwa Mkuu wa Wilaya kwa niaba ya madiwani wa kata za Ndala na Usanda, amemshukuru Dc Mboneko kwa juhudi zake za kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya elimu zikiwemo zile za upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati.
Wakiongea katika hafla hiyo, wakuu wa Shule za Sekondari Ndala, Ibinzamata na Shigita walimshukuru Mkuu wa Wilaya Mboneko kwa kuwapatia zawadi hizo za viti na meza za walimu na wakaahidi kuwa kwa mwaka huu watafanya vizuri zaidi.