Breaking

Friday, 4 March 2022

BIMA YA AFYA KWA WOTE NI KIPAUMBELE CHA SERIKALI – WAZIRI UMMY

 


Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa kipaumbele cha Serikali kupitia Wizara yake ni suala la Bima ya Afya kwa kila mwananchi ili kuondoa malalamiko ya upatikanaji wa huduma za matibabu.

Waziri Ummy ameyasema hayo wakati  akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita ya  Samia Suluhu Hassan.

Anesema kuwa Kipaumbele chake kikubwa katika Wizara hiyo ni kila mwananchi kuwa na bima ya afya kwani mwananchi anapokuwa na kadi ya bima ya afya anapata huduma za matibabu bila malalamiko yoyote kuliko mwananchi anayepata huduma bila kuwa na kadi.

Ametumia mfano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo asilimia 80 ya wagonjwa wake ni wanachama wa NHIF ambao wanapata huduma za matibabu bila ya kuwa na malalamiko yoyote.

“Serikali imeshawekeza sana katika sekta ya afya na kilichobaki kwa sasa ni kusimamia upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na upatikanaji wa bima ya afya ili kurahisisha huduma hizo, tunaamini suala la bima ya afya kwa wote lilipofikia ni pazuri na tutakwenda nalo bungeni mwezi Septemba ili sheria hii ianze kutumika,” alisema Mhe. Ummy.

Kwa upande wa NHIF ambayo kwa sasa inahudumia asilimia nane ya Watanzania wote, inaendelea na mpango wake wa kuwafikia wananchi wengi zaidi ili waweze kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu.

Mkurugenzi Mkuu Bwana Bernard Konga amesema kuwa, NHIF imeweka utaratibu kwa kila kundi na kila mwananchi unaomwezesha kujiunga na kunufaika na Mfuko umefanikiwa kuwa na mtandao mpana wa vituo vya kutolea huduma za matibabu Tanzania Bara na Zanzibar.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages