Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amezielekeza Taasisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Taasisi ya Hakimiliki nchini (COSOTA) kukamilisha zoezi la kuwasajili wasanii wote hususan wale wa kubwa ambao bado hawajasajiliwa huku akisisitiza kuwa hakuna msanii mkubwa kuliko nchi.
Waziri Mchengerwa ametumia muda wa takribani masaa matatu kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali hususan ya wasanii na kutoa maelekezo ya kusaidia wasanii wote nchini na kuwaunganisha ili waweze kufaidika na kazi zao alipokuwa mgeni rasmi kwenye kikao cha Baraza la wafanya kazi la Wizara yake Machi 21, jijini Dodoma.
“Leo nataka niwaelekeze BASATA na COSOTA na sitaki kurudia rudia jambo hili.Hatutegemei kusikia eti wamesajiliwa wasanii wachache, au kusikia msanii mkubwa hajasajiliwa tutaanza kuhoji uwezo wa wewe tuliokupa dhamana”. Amefafanua Mhe Mchengerwa
Amewafunda Watendaji wa Wizara na Taasisi zake kwa kuwataka kuwa wanyenyekevu na kutoa huduma kwa weledi na kuwasaidia wasanii kwa kuwa kupitia kazi zao wanatoa mchango mkubwa kwa nchi na Serikali inafaidika kwa kodi wanayoipata.
“Jukumu letu ni kuwaunganisha wasanii wote bila kujali anatoka kundi gani kwa kuwa hakuna msanii mkubwa kuliko nchi, kwa hiyo sisi tuliopewa mamlaka twende tukawanyenyekee wasanii hawa, wanatoa mchango mkubwa wa ajira, nchi yetu inanufaika kupitia kodi mbalimbali.Pia ni muhimu tukumbuke kwamba Wizara yetu inawagusa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wake”.Amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Amekemea tabia ya kujifungia maofisini kuwasubiri wasanii wawatafute na badala yake amewataka watendaji watoke na kuwafuata wasanii waliko ili wawasaidie.
Aidha amewataka kutoa elimu kwa wasanii ya mambo mbalimbali kama jinsi ya kujisajili na masuala mengine yanayowahusu ili wafanye kazi zao kwa rah ana kunufaika nazo.
Kuhusu kuwashirikisha wasanii kwenye ngazi mbalimbali za maamuzi Waziri Mchengerwa amewataka watendaji kutoa mapendekezo ya wajumbe wa bodi mbalimbali za tasnia za michezo na sanaa kwa wanamichezo na wasanii ili waweze kushiriki kikamilifu katika kusimamia biashara zao, kutafuta masoko na kulinda na kupigania haki zao moja kwa moja .
Akitolea mfano ya Wasanii wa Kenya akina Juakali amesema ndiyo wanaosimamia na kulinda haki zao ndiyo maana hawakubali sanaa ianguke kwa kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wameanguka wao.
Kwa upande mwingine Waziri Mchengerwa amewaagiza Wakuu wa Idara na Vitengo chini ya Wizara yake kusimamia kwa dhati suala la maadili ambapo amewahimiza kutumia muda wao wa kazi kuhudumia wananchi kwa kujibu hoja za wananchi na kutatua kero zao kwa haraka na ufanisi.
Amewataka watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi huku wakiongeza bidi kazini, uadilifu, uwajibikaji pamoja na kuzingatia sheria ambayo ndiyo misingi ya utendaji wa kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.