Breaking

Thursday 17 March 2022

AKAMATWA NA KETE 15 ZA MADAWA YA KULEVYA





Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linamshikilia Talib Ali Juma (22) kwa tuhuma za kupatikana na kete 15 za unga unaodhaniwa kuwa ni madawa ya kulevya na msokoto mmoja wa majani makavu yadhaniwayo kuwa ni bhangi baada ya kufanyiwa upekuzi katika nguo zake alizokua amezivaa.

Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Juma Khamis amesema kuwa mnamo Marchi 16, 2022 majira ya saa saba mchana katika kijiji cha Tumbe kitongoji cha Kojifa mtuhumiwa alipatikana na madawa hayo baada ya makachero waliokuwa doria maeneo hayo kumtilia mashaka kijana huyo na ndipo alipokamatwa na kufanyiwa upekuzi katika nguo zake alizokua amevaa na kisha kupatikana na kiasi hicho cha Madawa ya kulevya.

Kamanda Khamis amesema Upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa maandalizi ya kupeleka Kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kielelezo hicho kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na baadae jalada litapelekwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka na kisha Mahakamani.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limejipanga kuongeza misako na doria Sambamba na kuongeza operesheni maalumu kwa Wilaya ya Micheweni kutokana na uwepo wa bandari bubu nyingi unaosababisha wauzaji wa Madawa hayo kutumia Wilaya hiyo kuingiza madawa Mkoani hapa kwani kwa kipindi cha mwezi March pekee watu 4 wamekamatwa na madawa ya kulevya katika matukio matatu tofauti.

Aidha, ametoa wito kwa kuitaka jamii kuliunga mkono Jeshi lao la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kukamtwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya sambamba na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani ili jamii iishi kwa amani.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages