Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka watanzania wanaotumia usafiri wa bodaboda kuwa makini ili kupunguza ajali zinazopelekea kupoteza viungo vya mwili.
Ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 21, 2022 Wakati akifungua mafunzo ya wataalamu wa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo pamoja na wagonjwa mahututi yanayofanyika katika taasisi ya mifupa ya MOI jijini Dar es Salaam.
Waziri Ummy amesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati, kwa sababu Tanzania inashuhudia ongezeko la upasuaji wa mifupa, uti wa mgongo pamoja na magonjwa ya mishipa ya fahamu kutokana na ajali mbalimbali ikiwa ni pamoja na bodaboda.
"Sio jambo jema kwa Bodaboda kuanza kujifunza kuendesha pikipiki leo na kesho anaingia barabarani kuchukua abiria, ajali nyingi zinasababishwa na uzembe na kutofuata sheria za barabarani". Amesema Waziri Ummy.

"Tutakaa na wenzetu wa Wizara ya mambo ya ndani kuhakikisha tunatafuta ufumbuzi wa hili ili kupunguza ajali za uzembe zinazoweza kuepukika kwa kuwa watu wengi wamekuwa wakipoteza viungo vyao vya mwili kwa kuvunjika na kuwekewa vya bandia." Amesema Waziri Ummy.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na watanzania kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini Marekani, Australia pamoja na Canada na lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi, uzoefu na utaalamu.
.jpg)