Breaking

Saturday, 19 February 2022

WAZIRI MHAGAMA AWATAKA TPA KUWA WABUNIFU NA KUONGEZA MAPATO






WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuwa na ubunifu kiutendaji ambao utaongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato yatakayoiwezesha Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha huduma kwa wananchi.

Mhe. Jenista amesema kuwa, mapato yatakayopatikana kupitia bandari yatatumiwa na Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta zote muhimu zinazotoa huduma ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja.


“Mapato ya bandari zetu ndio yataiwezesha Serikali kuboresha huduma za afya, elimu, barabara na umeme kwa Watanzania,” Mhe. Jenista amefafanua.

Waziri Jenista amawataka watumishi wa TPA kutambua kuwa, wana umuhimu mkubwa katika ukuaji wa uchumi kwani ubunifu na nguvu kazi yao ina mchango mkubwa wa maendeleo ya taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo hawana budi kufanya kazi kwa bidii ili taifa linufaike na utumishi wao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Eric Hamissi amesema, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha, TPA imejiwekea malengo ya kukusanya shilingi trilioni moja ili kuiwezesha Serikali kutekeleza wajibu wake wa kuboresha huduma kwa wananchi.

“Itakapofika tarehe 30 Juni, 2022 tutakuwa tumekusanya shilingi trilioni moja, kwa mwendo tulionao nina imani tutafikia lengo kwani mpaka sasa ndani ya miezi saba, TPA imekusanya bilioni 610, hivyo kiasi cha shilingi bilioni 390 kilichobakia kitapatikana ndani ya miezi iliy
obaki,” Bw. Hamissi amesisitiza.

Baraza hilo pamoja na mambo mengine limepokea na kujadili Taarifa ya Kamati ya Utendaji pamoja na Bajeti pendekezwa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages