Breaking

Wednesday, 23 February 2022

WAMILIKI WA HOSPITALI BINAFSI MARUFUKU KUPOKEA WATUMISHI WA AFYA WA SERIKALI NDANI YA MUDA WA KAZI

Na WAF-MWANZA

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amepiga marufuku Wamiliki wa Hospitali Binafsi tabia ya kuwapokea Watumishi wa afya wa Serikali wakati wa muda unaowataka wawe katika vituo vyao vya Serikali. 

Dkt. Sichalwe ametoa agizo hilo leo Jumatano Februari 23, 2022 wakati akiongea na Wajumbe wa Bodi ya ushauri ya hospitali Binafsi, Wataalamu wa afya ngazi ya Mkoa, na Jiji pamoja na Wamiliki wa Hospitali Binafsi Jijini Mwanza. 

Amesema, Serikali haina lengo la kumkataza Mtoa huduma yoyote kufanya kazi katika vituo vya kutolea huduma binafsi, bali ni lazima utaratibu ufuatwe ili kuepuka changamoto ya upungufu wa Watoa huduma katika vituo vya Serikali wakati wa muda husika. 

"Ni marufuku kumpokea Mtumishi aliyeajiriwa na Serikali, ndani ya muda wa kazi wa Serikali, tukikupata hatutakuwa na huruma, kwasababu tunataka utaratibu ufuatwe Watumishi waje baada ya muda wa Serikali kumalizika." Amesema Dkt. Sichalwe. 


Mbali na hayo, Dkt Sichalwe amewaelekeza Wamiliki hao kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuanzia mgonjwa anapoingia getini, anapopata huduma mpaka anapoondoka ili kuondoa malalamiko yanayoweza kuzuilika. 

Sambamba na hilo, amewataka watoa huduma za afya kuepuka vitendo vya Rushwa na kufanya kazi kwa juhudi na weledi kulingana na taratibu na miongozo ya taaluma zao wakati wa kuwahudumia wananchi ili kuondoa uvunjifu wa haki na malalamiko yanayoweza kuzuilika. 

Aidha, amepiga marufuku vitendo vya kutoa dawa zikizopita muda kwa wagonjwa, huku akisisitiza Serikali imeanza kufuatilia hilo na watakaobainika watachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa watoa huduma wengine. 

"Wapo miongoni mwetu ambao sio waaminifu, utakuta dawa imepita muda wake lakini wanaendelea kuitoa kwa wagonjwa, na hii mara nyingi inatokana na utunzaji mbaya wa dawa hizo kwenye vyumba vya vya kuhifadhia dawa" Amesema. 



Mbali na hayo, Dkt. Sichalwe amewaelekeza kuhakikisha wanaajiri watumishi walio na vigezo na wanaotambulika na Mabaraza yao ili kuongeza tija katika kuboresha utoaji huduma kwa wananchi, hasa katika eneo la maabara, eneo la dawa na uzazi. 

Pia, Amewaelekeza kufuata Sheria na utaratibu, hasa katika ufunguaji wa Hospitali na Maabara ili kuepuka kuwa na Maabara bubu ambazo nyingi zinatoa huduma kwa viwango duni hivyo kumnyima fursa mwananchi kupata huduma bora za afya. 

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa amemshukuru Mganga Mkuu kwa kutenga muda na kuja kuongea na Wamiliki wa Hospitali Binafsi katika Mkoa wa Mwanza jambo litaloongeza tija katika kuboresha utoaji huduma kwa wananchi. 

Hata hivyo, amewakumbusha Wataalamu wa afya katika Mkoa huo hususan Madaktari kuhakikisha wanahuisha leseni zao kulingana na Sheria na taratibu za baraza lao ili kupata kibali cha kuendelea kutoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya. 

Mwisho.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages