Breaking

Wednesday, 23 February 2022

TCRA YAELEZA SABABU TATU ZA BANDO KUISHA HARAKA



Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetaja vitu vitatu vinavyosababisha kuisha kwa bando haraka ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa kasi ya internet, uwezo wa simu janja na kuwa na application nyingi kwenye simu.

Pia imesema gharama za kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine nchini ni nafuu ukilinganisha na nchi nyingine duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jabiri Bakari ameyasema hayo jana Jumanne Februari 22 wakati wa mkutano wake na Jukwaa la Wahariri nchini (TEF).

“Tafiti mbalimbali duniani zinaonyesha kuwa, gharama za kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine nchini Tanzania, zipo chini tofauti na nchi nyingine duniani, gharama za kawaida bila kujiunga na kifurushi, pamoja na gharama zilizounganishwa na kifurushi nazo zimeshuka,” amesema.

Amesema Tanzania inaongoza kwa kuwa na vifurushi rahisi na salama Afrika na duniani, hivyo kila mtoa huduma anauwezo wa kubadilisha vifurushi kila baada ya siku 90.

Mkurugenzi huyo amesema kabla vifurushi havijabadilishwa, mtoa huduma kuleta mapendekezo yake TCRA kwa ajili ya kuangalia kama inaendana na utafiti uliofanya ili kutomuumiza mlaji au mtumiaji wa huduma za mawasiliano nchini.


Amesema watumiaji wa simu janja nchini ni asilimia 27 ambao wanaonekana kutumia muda mdogo kusoma habari ndefu, hivyo wengi wanaotumia simu hizo hupoteza data bila kujua.

Naye Mkurugenzi Masuala ya Sekta TCRA, Dk Emmanue Manasseh akizungumzia kifurushi katika simu amesema kumekuwa kukisemwa kuwa vifurushi hivyo vinaisha kwa haraka lakini Mamlaka hiyo imekuwa ikifanya majaribio mbalimbali ili kuhakikisha watoa huduma wanatoa huduma sawa na walichowaahidi watumiaji.

Ametaja vitu vinavyosababisha kumaliza kifurushi kwa haraka kuwa ni kuongezeka kwa kasi ya mtandao kwenye simu janja mfano kutoka 3G hadi 4G.

Pia, ubora wa video na picha unavyoongezeka maana yake matumizi nayo yanaongezeka.

"Tuna “application” mbalimbali kwenye WhatsApp zinaboreshwa mara kwa mara nazo zinatumia data. Watumiaji wengi wa simu kuna vitu vinaendelea kwenye simu yake lakini mtumiaji hajui. Uwepo wa application nyingi, nyingine hazitumii hivyo zinamaliza bundle,” amesema.

Amesema TCRA imeelekeza watoa huduma kutengeneza ‘application’ ambazo watumiaji wanaweza kufuatilia matumizi yao.

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages