Breaking

Tuesday, 22 February 2022

RAIS SAMIA AFUNGUKA KUHUSU MAUAJI, ALIAGIZA JESHI LA POLISI KUSHIRIKIANA NA JAMII



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema sababu za Matukio ya Mauaji yanayoendelea Nchini zinaonesha Watu hawako karibu na Mungu, kwani hakuna Dini iliyotoa ruhusa kujiua au kuua.

Rais Samia Amesema hayo leo Jumanne Februari 22, 2022 katika sherehe za Jubilee ya miaka 25 ya Askofu Severine Niwemugizi iliyofanyika wilayani Ngara mkoani Kagera.

Amesema kuwa yanapotokea mauaji Serikali huwa inaunda Tume ndani ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi na Ripoti zinapokuja huonesha sababu mbalimbali ya mauaji hayo  ikiwemo wivu wa mapenzi, ugumu wa maisha na imani za kishirikina. 

Amesema kuwa sababu hizo zinakuonesha kuwa watu hawako karibu na Mungu kwani hakuna dini inayoruhusu kufanya mauaji.

"Tunaambiwa anayetia uhai na anayetoa uhai ni Mungu peke yake, na tunafunzwa kuamini kwamba kifo kinapotokea ni kazi ya Mungu sasa sina hakika wanaojiua au kwenda kuua wenzao kama ni kazi ya Mungu" Rais Samia Suluhu Hassan

"Kumekuwa na matukio mengi ya mauaji na watu kujiua. Takwimu zinaonesha katika wilaya ya Ngara pekee mwaka 2020 kulikuwa na matukio 22 ya mauaji, Mwaka 2021 (21), Mwaka 2020 kulikuwa na matukio matatu ya watu kujiua na mwaka 2021 matukio mawili" ameongeza 

Aidha ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini na machief  katika kukabiliana na mauaji na watu kujiua.

Katika hatua nyingine Rais Samia 
amesema hana tabia ya kutukuzwa wala kulinganishwa na Mungu na kuwa atajitahidi kuwa na hekima na uvumilivu wa kusikiliza maoni ya wengine.

Alikuwa akijibu kauli iliyotolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi aliyeemuomba Rais Samia kutokubali kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile.

Askofu Niwemugizi Alisema “Nikikuombea uwe na afya njema na uwe mnyenyekevu lakini pamoja na madaraka hayo makubwa uliyonayo usikubali kamwe kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile usikubali."

"Ninakumbuka sana Hayati Benjamini Mkapa najua huko mlikuwa mmezoea mtukufu rais, mtukufu rais alifika mahali akawa mkali kabisa mtukufu ni Mungu tu naomba hilo liwe neno kwako, " amesema Askofu Niwemuguzi.

Akijibu kauli hiyo Rais Samia amesema “Baba Askofu katika kufunga hotuba yako umeniasa mambo ya kukataa kutukuzwa na mimi nataka nikuahidi mbele ya umma huu kwamba, hii si tabia yangu na ninajitahidi kujishusha niwe sawa na wengine. Maana utumishi huu kama mipango ya Mungu ilivyo ameniweka hapa niwatumikie na siyo nijitukuze kwenu kwahiyo nitawatumikia,”

Ameongeza kuwa atajitahidi kuwa na hekima na uvumilivu na awe na sikio la kusikiliza yale yanayosemwa na wengine.

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages