Akizungumza leo Jumapili Februari 20, 2022 katika hafla ya kuwakaribisha wananchama hao iliyofanyika Makao makuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam, Masoud Hamad Masoud amesema sababu ya kurudi CUF ni kuandamwa na makada wa chama hicho tangu alipotangaza nia ya kugombea wadhifa huo ambao Juma Haji Duni alishinda.
Amesema kuwa kama kungelikuwa na uchaguzi huru, haki na demokrasia katika uchaguzi wa Uenyekiti Taifa wa Chama cha Act Wazalendo angemshinda Juma Duni na asingepata hata asilimia 20.
"Waliona Hamad akiwa mwenyekiti ni mwiba walifanya mambo mengi wanayoyajua ikiwemo Kamati yote ilikuwa inanipinga. Nafikiri Mimi hata kama ningeshinda nisingeweza kufanya Kazi peke yangu kwa sababu kamati yote ilikuwa hainiungi mkono," amesema.
"Niliwahi kuwa Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi Zanzibar nilijiuzulu kwa sababu meli ilizama na iliua watu wengi, sikuwa kepteni wala nahodha. Nilijiuzulu kwa lengo la kulinda heshima na chama changu hata uchaguzi ule sikuona haki pale," amesema.
Masoud ameitaka ACT Wazalendo kurudisha ofisi zote wanazofanyia Zanzibar kwa kuwa ofisi hizo zilijengwa kwa michango ya wananchama wa CUF.
Aidha, amesema yeye na kundi lake wanaenda Unguja na Pemba kurejesha ofisi zao ambazo zilichukuliwa na ACT na kukitaka chama cha ACT wajipange kupoteza wanachama kwa kasi kubwa.
“Ukiona maskini anakula kuku, ama kuku mgonjwa au maskini mgonjwa, ng’ombe hachinjwi mkiani anachinjwa shingoni. Nimejipanga kupandisha bendera za CUF kila ambapo panahitajika kufanyika ili kurejesha chama hiki kwenye hadhi yake,” amesema.
Awali akiwakaribisha wanachama hao, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba amesema watapangiwa majukumu ya kukijenga chama hicho.
“Nawashukuru kwa kurudi nyumbani sehemu ambayo haki inapiganiwa na nitoe wito kwa wengine warejee CUF, waje washike nafasi za uongozi hasa Zanzibar.
“Wengine hasa mimi umri wangu umeshakwenda, tunahitaji vijana waje waunganishe nguvu kuendelea mapambano ya kupigania haki sawa kwa wote,” amesema Profesa Lipumba.
“Nawashukuru kwa kurudi nyumbani sehemu ambayo haki inapiganiwa na nitoe wito kwa wengine warejee CUF, waje washike nafasi za uongozi hasa Zanzibar.
“Wengine hasa mimi umri wangu umeshakwenda, tunahitaji vijana waje waunganishe nguvu kuendelea mapambano ya kupigania haki sawa kwa wote,” amesema Profesa Lipumba.
Miongoni mwa wanachama waliotambulishwa kutoka CCM, Chadema na ACT Wazalendo, 133 ni kutoka Tanzania Bara na 71 kutoka visiwani Zanzibar.