Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma mkoani Mara imemhukumu kifungo cha miaka 60 jela mtu mmoja aitwaye Daud Nyamwela Samson (22) mkazi wa Bwai baada ya kumkuta na hatia ya makosa mawili ya kumlawiti na kumbaka bibi wa miaka 56 mkazi wa Bwai Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara.
Hukumu ya kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021 imetolewa leo Februari 23, 2022 na Hakimu Stanly Mwakihaba baada ya kujiridhisha na mashahidi watano wa upande wa Jamhuri pasipo kuacha shaka yoyote katika shauri hilo.
Daudi Nyamwela ametiwa hatiani baada ya kukukwa na hatia ya makosa mawili tofauti aliyotenda Desemba 25, 2021 ambapo alimvizia bibi huyo katika kichaka wakati akienda msibani na ndipo akambaka na kisha kumlawiti na kumvunja mgongo akiwa na kisu na kwamba, bibi huyo alipojaribu kumhoji kwa nini anambaka na kumwingilia kinyume cha maumbile yake alimwambia atamchoma kisu alichokuwa nacho mkononi.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwakihaba amesema kwamba kulingana na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri mtuhumiwa ametiwa hatiani kwa makosa mawili tofauti, ambapo kosa la Kwanza ni kumbaka bibi huyo kwa kikiuka kifungu cha 130 (1), na( 2) b, pamoja na kifungu cha 131( 1 ) ambapo adhabu yake ni miaka 30 jela.
Pia, mtuhumiwa ametiwa hatiani katika kosa la pili la ulawiti na kumvunja mgongo bibi huyo kinyume cha kifungu cha 154 (i) (a), ( ii ) (2) vya sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2009 ambapo adhabu yake ni miaka 30 jela.
Aidha, Hakimu Mwakihaba kabla hajasoma humumu ya adhabu hiyo alimpa fursa mtuhumiwa ya kujitetea ambapo hata hivyo mtuhumiwa hakusema chochote badala yake alikaa kimya akitazama chini.
Awali Wakili wa Serikali, Tawabu Yahya Issa aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa Jamii katika kuhakikisha vitendo hivyo vinamalizika.
Katika hatua nyingine, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma inawatafuta watu wawili ambao ni Nyanjala Mulungu na Julias Mataro wakazi wa Kigera Etuma ambao walimwekea dhamana kila mmoja ya shilingi milioni 10 mtuhumiwa wa ubakaji aitwaye Mtawa Julias Mgoli ambaye alimbaka mwanafunzi anayesoma katika shule moja ya manispaa ya Musoma (jina la shule limehifadhiwa).
Mtuhumiwa wa kesi hiyo namba 100 ya mwaka 2020, ataanza kutumikia kifungo chake cha Miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani na Mahakama hiyo pasipo kuacha shaka yoyote ile.
Source DIRAMAKINI